Pages

RAIS DKT. MAGUFULI AENDELEA NA ZIARA YAKE KATIKA WILAYA ZA IGUNGA NA NZEGA MKOANI TABORA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanga Wilaya ya Igunga Ndugu
Masesa Kishiwa Makala kutoka Chadema wakati akiwa safarini kuelekea
Nzega Mkoani Tabora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiwasalimia wakazi wa Ziba Wilayani Igunga mkoani Tabora hawaonekani
pichani wakati akielekea Nzega Mkoani Tabora.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na  wabunge wa Mkoa wa Singida wakati akiwahutubia wakazi wa Misigiri Mkoani Singida wakati akiwa njiani kuelekea Mkoani Tabora.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wakazi wa Misigiri Mkoani Singida. PICHA NA IKULU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe  30 Julai, 2016 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tabora akitokea  Mkoa wa Singida.

Kabla ya kuingia Mkoani Tabora, Rais Magufuli  amezungumza na wananchi wa Mji wa Misigiri katika Wilaya ya Iramba  ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida  kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara  moja kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.

Rais Magufuli amesema  serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna  sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.Mkoani Tabora, Rais Magufuli  amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya  Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na  Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha  inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea
malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na  soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kituo cha
mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu
ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.

Kuhusu kero ya maji, Dkt.  Magufuli amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za kimarekani Milioni 268.35 kutoka nchini India ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya ziwa Viktoria katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni moja na laki moja (1,100,000)  watanufaika.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo  Serikali imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza  mradi wa kusambaza maji ya kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji ya  Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa  bomba kuu ambako watu laki sita (600,000) watanufaika.

Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.

"Ninapenda tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu
masikini, mtu ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano
halafu nyinyi mnamtoza kodi."Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa watu
wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu
mnyonge mwenye gunia moja" Amesema Rais Magufuli.


Kuhusu maombi ya Mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na  ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais Magufuli amesema haioni umuhimu wa  kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa, na badala yake fedha  zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara,
miundombinu na huduma za afya.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Nzega
30 Julai, 2016 

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)