Pages

Msama afichua mtandao wa wizi wa stika za TRA

Mkurugenzi wa Msama Action Mart, Alex Msama akionesha stika za TRA pamoja na CD feki ya mwimbaji wa nyimbo za injili Boniphace Mwaitege lakini imewekwa stika ya TRA wakati wa mkutano na  waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
(Na Mpigapicha Wetu)


NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Msama Action Mart ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama amewalaumu baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhujumu mapato halali ya waimbaji, wasanii na Serikali.

Msama alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, baadhi ya maofisa hao wa TRA, wamekuwa wakiuza ‘stika’ kwa wezi wa kazi za waimbaji na wasanii ili ‘kutakatisha’ kazi za wizi.

“Unakamata CD feki, lakini unakuta ina ‘stika’ ya TRA. Unajiuliza inakuweje?  Yote hii ni kutokana na baadhi ya maofisa wa TRA kuuza ‘stika’ hizi isivyohalali kwa wezi,” alisema huku akionesha mfano wa stika halali na CD feki.

Msama, mmoja wa wadau wa vita dhidi ya wizi wa kazi za waimbaji injili na wasanii, alisema wanachofanya wezi  ni kubandika ‘stika’ halali katika kazi feki  na kuziuza.

“Hawa jamaa wamebuni mbinu mpya ya kutumia stika halali za TRA katika kazi feki, jambo ambalo linahitaji uzoefu kubaini kwamba ni feki,” alisema Msama.

Alisema hujuma hiyo dhidi ya jasho la waimbaji na wasanii, imekuwa ikiwanyima wahusika kufaidi jasho la kazi zao kwani huishia kwa wajanja hao wachache. “Kama si dili ya baadhi ya maofisa wasio waaminifu wa TRA, wezi hawa wangepata wapi stika hizo? alihoji Msama huku akionyesha stika halali za TRA na CD feki.

Alisema kibaya zaidi ni kwamba, stika hizo feki hazitumiki kwa kazi hizo feki za waimbaji na wasanii, pia hata kwa bidhaa nyingine ili kuzihalalisha.

Msama anatoa wito kwa jamii kusaidia vita hiyo ngumu kwa kuacha kununua kazi feki ili kuinua uchumi wa wasanii na nchi kwa ujumla.

Alisema vitendo hivyo vya baadhi ya maofisa wasio na uadilifu, vinarudisha nyuma harakati za Serikali kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Msama ametoa wito kwa uongozi wa TRA kufanya kila uwezalo kuwabaini maofisa hao wenye kukiuka maadili ya kazi yao kwani wanakipaka matope chombo hicho.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)