Pages

DKT. REGINALD MENGI AMTUMIA UJUMBE MZITO WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA

Katika kufikia malengo ya Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi amemtumia Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ujumbe kupitia kwa Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu Mh. Jenista Mhagama, ujumbe ambao anaamini kama ukifanyiwa kazi Tanzania itaweza kufikia malengo yake kwa haraka zaidi.
Dkt. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa makampuni ya IPP alituma ujumbe huo kwa Waziri Mkuu wakati ufunguzi wa Kongamano la Mashauriano ya Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji ambalo linafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, kongamano lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Alisema kuwa pamoja na serikali kufanya jitihada nyingi ili kuwashirikisha wananchi wake katika uwekezaji kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi lakini bado kuna changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikijitokeza na zinahitaji kufanyiwa kazi.

Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza katika Kongamano la Mashauriano ya Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji kwa niaba ya TPSF ambapo alitumia fursa hiyo kuishauri serikali mambo ambayo anaamini serikali ikiyafanyia kazi uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi tofauti na sasa.(Picha na Modewjiblog)

"Serikali imekuwa ikitumia pesa kuwapeleka vijana kusoma nje lakini nikakutana na kijana mmoja akaniambia kasoma nje lakini bado hana ajira na alipelekwa kusomea digrii ya mambo ya mafuta na gesi,

"Nadhani ni vyema serikali ikabidili mwenendo wake na kuhakikisha vijana wote ambao wanapelekwa kusoma nje wakirudi nchini wapewe nafasi za kazi ili kulisaidia taifa kwa hiyo naomba utufikishie ujumbe kwa Waziri Mkuu ukienda Dodoma katika mkutano mkuu wa chama," alisema Dkt. Mengi.

Pia alisema nchi yetu imekuwa ikitegemea zaidi kilimo hivyo iwekeze katika kilimo na iache kuagiza nje bidhaa ambazo zinatengenezwa na vyakula ambavyo vinapatikana nchini lakini pia kuwapa vipaumbele wawekezaji wazawa na hata wanapokuja wageni ihakikishe na watanzania wanashiriki kikamilifu katika kuwekeza.

Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza katika Kongamano la Mashauriano ya Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

"Nchi yetu kwa miaka mingi tunajulikana kuwa tunafanya zaidi kilimo na nadhani hapa kunahitaji ushirikishwaji mkubwa wa watanzania na tuache kulima nanasi na hapo hapo tunaagiza juisi ya nanasi nje ni muhimu watanzania watambue kuwa nchi yao ni tajiri na wakishiriki kikamilifu itafika mbali," alisema Dk. Mengi.

Kwa upande wa Waziri Mhagama ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi alikiri kuwepo kwa baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lakini serikali inalifahamu hilo na wameanza kufanya mabadiliko ya sheria na sera wanazozitumia kwa sasa.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu Mh. Jenista Mhagama akitoa hotuba katika kongamano hilo pamoja na kujibu baadhi ya hoja alizotoa Dkt. Mengi.

"Serikali inalifahamu jambo hilo kama kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ili kuwasaidia Watanzania kukuza uchumi wao na wa taifa, kwa sasa tumeanza kufanya mabadiliko kwa baadhi ya sheria na sera na tutaendelea kuangalia ni wapi kunahitajika mabadiliko ili kila jambo lifanyike kwa faida ya watanzania wote," alisema Waziri Mhagama.

Akielezea kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng`i Issa alisema malengo ya kongamano ni kubadilishana mawazo na wadau mbalimbali wa serikali na sekta binafsi lakini pia kushirikisha mashirika ya nje ya nchi ili kuweza kupata njia bora ambayo itakwenda kutumika katika kuwashikirikisha watanzania wote ili kila mmoja ashiriki kukuza uchumi wa taifa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng`i Issa akielezea malengo ya kongamano hilo la siku mbili.

Baadhi ya wageni waalikwa ambao wamehudhuria kongamano hilo la siku mbili.



Wageni rasmi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kongamano.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)