Pages

Imelda Myovela:Mwanamke pekee fundi wa umeme kiwanda cha TBL Arusha

Imelda akiwa  akiwa kazini

-Ashauri wanawake kuchangamkia masomo ya ufundi

“Tatizo la ajira nchini limekuwa likiongezeka hapa nchini mwaka hadi mwaka ila wanawake wengi ndio hawana kazi wameachwa nyuma katika sekta zote kiasi kwamba kunahitajika ushawishi wa ziada wa kuwahimiza watoto wa kike nchini kuachana na kasumba ya kuchagua kazi”Anasema Imelda Myovela ,mfanyakazi wa kiwanda cha TBL Arusha ambaye ni mwanamke pekee fundi wa umeme.

Myovela anaendelea kueleza kuwa iwapo watoto wa kike hawatapata ushawishi wa kuwaeleza kuwa masomo yote wanayaweza wanapokuwa mashuleni na wana uwezo wa kufanya kazi yoyote inayofanywa na wanaume kuna hatari ya wanawake wa Tanzania kuendelea kubaki nyuma kwa kuachwa nje ya mfumo wa ajira.

Alisema jambo la kusikitisha hata watoto wa kike wengi wanaosoma masomo ya ufundi mara nyingi wanabadilisha kazi na wengine kuamua kukaa bila kazi kwa kuogopa kufanya kazi walizosomea na hali hiyo ndio inasababisha kila sehemu ya kazi hususani za kawaida kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaume.

Akielezea historia ya elimu yake Imelda anasema baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari mwanzoni mwa miaka ya  themanini alijiunga na Chuo cha VETA cha Dar es Salaam ambapo alisoma kozi ya ufundi wa umeme wa viwandani.

Baada ya kuhitimu kozi hiyo na kufanya mafunzo ya vitendo,mwaka 1983 alifanikiwa kupata ajira katika kampuni ya TBL ya Dar es Salaam ambako ameajiriwa kama fundi umeme hadi kufikia sasa.
“Kufanya kazi katika kampuni hii kumeniwezesha kuwa na ujuzi mkubwa katika fani hii ikizingatiwa kuwa kuna mafunzo mengi tunapata ambayo huwezi kuyapata chuoni pia kampuni imefunga mitambo ya kisasa na inayotumia teknolojia ya juu hivyo inahitaji uwe umebobea katika fani kwendana na mazingira ya kazi”.Alisema.

Aliongeza kwamba anajivunia kazi yake japo wenzake wote anaofanya nao kazi ni wanaume na anafurahi kuona anaimudu na anaaminiwa na mwajiri wake kama wanavyoaminiwa wafanyakazi wanaume.

 Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo kwenye kazi nyingine . “Hakuna kazi isiyokuwa na changamoto kwa kazi kama hii ya kwangu unapokuwa na watoto wadogo na kufanya kazi za shift unakuwa na wasiwasi hata hivyo namshukuru mme wangu ni muelewa amekuwa akinisaidia na kunitia moyo”.Alisema
Imelda ambaye ni mama mwenye  watoto watatu anasema kuwa anafurahi kufanya kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye maslahi mazuri ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wafanyakazi wake  na anakiri kuwa ajira yake imemwezesha kupata mafanikio kimaisha mojawapo ikiwa ni kuwasomesha watoto wake kwenye shule nzuri .

“Kwenye kampuni kama hizi  tunafundishwa mambo mengi ambayo hata yanakunufaisha ukiwa nyumbani kwako kama vile usafi wa mazingira pia kupanga bajeti kwa kila kitu unachofanya”.Alisema

Kuhusu mipago yake ya baadaye alisema kwa sasa hana mpango wa kubadilisha kazi na itakapofikia wakati wa kustaafu ataendelea kufanya shuhuli zake binafsi za kujiajiri.


 Alimalizia kwa kuwataka akina mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake peke yao na hakua kazi rahisi kila kazi ina changamoto zake. “Akina mama tuamke na watoto wa kike changamkieni  masomo ya ufundi ili muweze kupata ajira nzuri zitakazowawezesha kuboresha maisha yenu”.Alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)