Pages

Kwa Fowadi hii ya Wachezaji wa Genk? Mbwana Samatta Labda Arogwe

Samatta ameikuta Genk ina mastraika saba kutoka Uturuki, Jamaica, Ugiriki, Georgia na wazawa wa Ubelgiji.

KWA mwanetu Mbwana Samatta tunayemjua na kwa Genk hii aliyokwenda,  labda alogwe. Lakini hakuna kitakachomzuia kuingia kwenye kikosi cha kwanza baada ya jana Ijumaa jioni kusaini mkataba wa miaka minne ambao unaanzia 2016-2020 mwaka ambao Rais John Magufuli atakuwa anatimiza miaka mitano ya kuongoza nchi.

Samatta ameikuta Genk ina mastraika saba kutoka Uturuki, Jamaica, Ugiriki, Georgia na wazawa wa Ubelgiji.

Huyo straika wa Uturuki anaitwa Enes Unal ni mchezaji wa Manchester City ya England ambaye ameletwa Genk kwa mkopo wa misimu miwili huu ni msimu wake wa kwanza na amepachika bao moja tu katika mechi zaidi ya 10 alizocheza.

 Huyo wa Georgia ni jamaa mmoja mtata sana uwanjani anaitwa Nikolaos Karelis anatumia guu la kushoto, mpaka sasa amefunga bao moja tu.

Sasa kuna mashine zao mbili wanazoziaminia ijapokuwa kiuhalisia umri umewatupa. Mmoja anaitwa Igor Alberto Camargo ana miaka 32, huyu jamaa amefunga mabao matano tu katika mechi zote 23 alizocheza.

Ni Mbrazili aliyepewa uraia wa Ubelgiji. Hao wangapi? Staa mwingine ni kibabu pia ana miaka 34 wanamuita Thomas Buffel ni pande fulani la mtu amefunga mabao matatu. Huyo wa Jamaica anaitwa Leon Bailey ni bwana mdogo kuliko hata Samatta, yeye ana mabao matatu.

Hao mafowadi wengine wala hata usitake kuwajua utakuwa unapoteza muda wako tu. Ila kwa jinsi Samatta alivyopania lazima mtu aende benchi.Sikia sasa mastraika saba wa Genk kwa ujumla wao katika mechi zote 23 walizocheza wamefunga mabao 12. Buffel na Camargo wamefunga mabao manane kati ya hayo. Ukiangalia takwimu hizo za mabao unapata jibu la kwanini Kocha Mbelgiji, Peter Maes alimtaka Samatta kwa nguvu zote kuokoa kibarua chake. Genk ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi ikiwa pointi 32, huku AA Gent wakiongoza msimamo kwa pointi 49.

Kwenye timu hiyo kuna Wakongomani wanne ambao wamezaliwa Ubelgiji wana uraia wa nchi mbalimbali. Wakongomani hao ni Derick Katuku Tshimanga ambaye ni beki wa kushoto anayetumia mguu wa kulia mwenye kilo 68 ana miaka 27.

Mwingine ni Christian Kabasele ambaye ni bonge la beki anatumia guu la kulia na kwa sasa amepachika mabao mawili kwenye ligi. Kuna Mkongo Mwingine anaitwa Neesken Kebano ni kiungo ana mabao matatu msimu huu.

Kuna Mnigeria anaitwa Onyinye Ndidi ni beki fulani mjanja mjanja mwenye bao moja. Yule Mghana Bennard Kumordzi ni beki. Wachezaji hao wameshazoea mazingira kwenye kikosi hicho na huenda wakawa msaada mkubwa kwa Mbwana Samatta ambaye jana Ijumaa alitaraji kufanyiwa vipimo vya afya pamoja na TP Mazembe kumalizana na Genk.

TP Mazembe jana ilikuwa kwenye mishemishe za kumalizana na Genk na kupokea dau lao la zaidi ya Sh.1.8 bilioni ambapo Simba wanasubiri mgao wao kutoka hapo. Klabu ya Genk  baada ya kushiriki Ligi ya Mabingwa mwaka 2012 iliwauza kipa wa sasa wa Chelsea, Thibaut Courtois na  Kevin De Bruyne ambaye pia alienda Chelsea kabla ya kutua Man City. Ilimuuza pia Christian Benteke kwa Aston Villa, sasa yuko Liverpool.Crdt Mwanaharakati Mzalendo Blog

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)