Pages

Symphorose Mhanza-Mwanamke fundi na mwendesha mitambo pekee kiwanda cha Konyagi

 
 Bi Symphorose Mhanza akiwa kazini katika kiwanda cha konyagi
Bi Symphorose Mhanza akitoa mafunzo ya uzalishaji kwa wafanyakazi wenzake  katika kiwanda cha konyagi kilichopo jijini Dar es Salaam


Ukifika katika kiwada cha Konyangi kilichopo eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kumkuta Bi.Symphorose Mhanza akiwa mitamboni huwezi kuamini kama ni mwanamke kutokana na anavyomudu kazi yake ya ufundi na uendeshaji mitambo.

Symphorose anasema kuwa japo kazi hii inaonekana kuwa ngumu kwa kuwa kuna wakati inabidi kutumia nguvu nyingi kama ilivyo desturi ya kazi za ufundi lakini ameizoea  na anaipenda.

“Naipenda sana kazi yangu na nimeizoea japo inaonekana  kuwa ni ngumu na inafanywa zaidi na wanaume lakini mimi naona kawaida japo sijaona mwanamke mwingine anayethubutu kuifanya kiwandani hapa”.Anasema.
Bi.Symphorose anasema  jambo linalompa faraja  kubwa na kuipenda zaidi kazi yake  ni kutokana na jinsi anavyoaminiwa na mabosi wake kiasi kwamba japo ni mwanamke peke yake katika kiwanda hicho anayefanya kazi hii lakini anathaminiwa na kuaminiwa kama wanavyoaminiwa wafanyakazi wenzake wanaume.

Akieleza historia yake ya kazi alisema mwanzoni mwa miaka ya tisini ndipo alipojiunga na kiwada cha Konyagi ambacho hivi sasa kiko chini ya kampuni ya TBL “Wakati huo ulipokuwa unaajiriwa ulikuwa kwanza unapata mafunzo ya ndani yaliyokuwa yanatolewa kweye fani mbalimbali ambapo mimi nilijifunza ufundi na uendeshaji mashine (Machine Operator) kwa kipindi cha mwaka mmoja na nilipofuzu ndipo nikaanza kuifanya kazi hii”.Anasema.

Bi.Symphorose aliendelea kueleza kuwa baada ya kiwanda hicho kubinafsishwa kuna mifumo mingi mipya imeanzishwa ikiwemo mafunzo ya mara kwa mara ambayo anadai yamesaidia kumpatia ujuzi mkubwa katika fani ya ufundi na uendeshaji mashine na kumjengea uwezo wa kujiamini zaidi.

Alisema anajivunia kufanya kazi katika kampuni hii hasa kwa jinsi alivyoweza kupata ujuzi mkubwa ambao unamuwezesha kumudu maisha popote atakapokwenda hata baada ya kustaafu kazi na kuamua kuendesha shughuli zake.

Kuhusiana na changamoto zilizopo katika kazi yake alisema ni za kawaida kama zilivyo katika kazi nyingine “Changamoto kubwa ni mabadiliko ya kiteknolojia ambayo ili kwenda  nayo sambamba inabidi uwe na ufuatiliaji wa mambo mbalimbali katika fani ya ufundi bila hivyo unaweza kuachwa nyuma kwa kuwa kila kukicha inabuniwa mitambo ya kisasa zaidi”.Alisema.
Kuhusiana na mafanikio ambayo ameyapata kutokana na  kazi yake Bi.Symphorose ambaye ni mama wa familia  mwenye  watoto anasema yapo mafanikio kwa kuwa anaweza kuchangia katika pato la familia katika kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto wake.

Mafanikio mengine ni kufundishwa na mwajiri wake mambo  mbalimbali  ambayo yanasaidia katika maisha ya kawaida “Hapa tunajifunza usafi wa mazingira,nidhamu ya kutunza fedha,kupanga bajeti,kuzingatia muda na mambo mengineyo mengi ambayo yanaweza kukusaidia sehemu yoyote katika maisha na ndio maana najivunia kufanya kazi kampuni kubwa kama TBL”.Alisema.

Alimalizia kutoa ushauri kwa watanzania wote kuwa tuachane na uzembe na tufanye kazi kwa bidii popote pale tutakapokuwa  tutafanikiwa na pia alishauri wanawake wenzake kuchangamkia fursa za ajira zitazojitokeza ili kuweza kupata kipato na kuwakwamua katika janga la umaskini.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)