Pages

Ombi la Dart kupandisha Nauli ya mabasi yaendayo Kasi, Mwanafunzi kulipa nauli ya mtu mzima

UDART waendeshaji wa huduma ya mabasi yaendayo haraka (Dar Rapid Transport) yatakayoanza kutoa huduma hiyo tarehe 10/01/2016 wamepeleka maombi kwa SUMATRA kuomba iidhinishiwe gharama ya usafiri jijini Dar iwe ni Tsh 1,200/- njia kuu (Morogoro Road) ambayo kimsingi ni kutoka Kimara hadi Posta na Tsh 700/- njia za pembeni (feeder roads) ambayo ni kutoka hapo ulipo pembezoni kwenda njia kuu (main route).

Mwanafunzi ni nusu nauli ya mtu mzima (Yani wanafunzi watalipa Sh.700 kwa njia kuu na Sh.350 njia za pembeni kutoka Sh.200 wanayolipa kwa sasa). Hii ni gharama kubwa sana kuimudu.

Kama ilivyo ada SUMATRA wameitisha mkutano wa wadau tarehe 05/01/2016 katika ukumbi wa Karimjee Hall saa tatu na nusu asubuhi ili kujadili na kupitisha nauli hiyo.

Tukumbuke kwamba toka awali tuliambiwa ujio wa mabasi hayo utarahisisha uharaka wa safari na kupunguza gharama za usafiri (nauli) na gharama za usafirishaji (mafuta na vipuri) kwa sababu hautakuwa na foleni kama ilivyosasa ambapo wasafirishaji (daladala) hulazimika kutumia gharama kubwa sana kwa safari moja.

Kwa sasa daladala zetu hizi mtu akiwa na Sh. 1,000/- anaweza kusafiri safari moja (barabara kuu 500/-) na safari nyingine (400) njia ya pembeni akatumia Sh. 100/- kula karanga.

Kama tozo hizi zilizopo sasa zilipangwa kulingana na mazingira magumu ya usafirishaji katika jiji la Dar es Salaam tunatarajia kuanza kutumika kwa miundombinu ya DART kutapunguza gharama za uendeshaji (mafuta na vipuri), kutaleta uharaka na pia kutapunguza gharama za usafiri (nauli) na sio kuziongeza.

Ombi langu kwenu:

Tarehe 05/01/2016 tujitokeze kwa wingi pale Karimjee Hall kiasi cha ukumbi kutapika. Yeyote anayedhani anaguswa na suala la usafiri Dar asibaki nyumbani. Tuifanye siku hii kuwa Bunge Huru la Dar.

Wananchi, Wanasiasa, Wanafunzi Vyuo Vikuu, Mama Ntilie, Wafanyakazi Viwandani, Machinga, Walimu, Wanafunzi, Wakwezi, Wavujajasho, Walalahoi, Wachumiajuani, Wavimbamacho, Walalapuu na Wadau wote wa usafiri wa umma tunaomba mjitokeze kwa wingi wenu kuja kupaza sauti za HAPANA.

Tukatae gharama hii ni KUBWA mno wala tusiingie mtego huu. Nauli ya 1200 kwa 700 ni kubwa sana na inamuumiza Mtanzania maskini anayetegemea usafiri wa daladala.

Hebu fikiria mama anayekaa Kimara anasafiri kila siku kwenda Soko la Samaki Feri kununua Samaki aje akaange auze apate vijisent vya kuendesha maisha yake na wanae. Kwa nauli ya sasa anatumia Sh.6000 tu kwa wiki nzima (yani 500/= × 2 ×6).

Lakini kwa nauli ya mabasi yaendayo haraka (DART) atalazimika kutumia Tsh 14,400 kwa wiki (yani 1200/= × 2 x 6). Ongezeko la Sh.10,800/= sawa na asilimia 140%.

Hili ni ongezeko kubwa sana ambalo watanzania maskini wanaotegemea usafiri wa daladala hawawezi kumudu. Ni lazima gharama hizi zishuke la sivyo watuachie daladala zetu zitumie hiyo miundombinu ya barabara za DART kwa gharama za sasa.

Tukiungana kwa umoja wetu tutashinda nguvu ya mabepari  wanaotaka kutumia umasikini wetu kutajirika maradufu. Mabasi haya ni mapya, barabara ni mpya hakuna sababu ya kupandisha nauli kwa kiasi hicho.

Vijana wenye uzalendo na nchi hii, kinamama, na wazee msilale jitokezeni tukawapiganie wananchi maskini wa nchi hii. Tarehe 05/01/2016 tukusanyike kwa wingi pale Karimjee Hall kupinga nauli hizi za kinyonyaji.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)