Meneja Mwendeshaji wa Taasisi ya MO Dewji, Francesca Tettamanzi (kulia) akitoa neno la ukaribisho kwa uongozi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha inayohudumia watoto wenye kansa nchini na waandishi wa habari katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa fedha kwa ajili ya watoto wenye kansa iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za MeTL Group jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mmoja wa Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha, Gerard Mongera na Wa pili kushoto ni Ofisa anayesimamia utekelezaji wa Programu wa Taasisi ya Tumaini la Maisha , Lilian Ndyetabula.
Afisa Mahusiano wa Taasisi ya MO Dewji, Zainul Mzige (kulia) akisoma taarifa kuhusu madhumuni ya kuanzishwa kwa MO Dewji Foundation pamoja na kazi wanazofanya katika kusaidia jamii ikiwemo sekta ya Afya na Elimu.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha, Gerard Mongera (kushoto) akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa MO Dewji Foundation na kuwaomba kuendelea kushirikiana nao wakati wa hafla ya kukabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 110 kwa ajili ya kusaidia watoto wenye kansa wanaohudumiwa na taasisi hiyo.
Meneja Mwendeshaji wa Taasisi ya MO Dewji, Francesca Tettamanzi (kulia) akikabidhi mfano hundi ya Shilingi Milioni 110 kwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha inayohudumia watoto wenye kansa nchini, Gerard Mongera (wa pili kushoto) kwa ajili ya kusaidia watoto wenye kansa wanaopata matibabu yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kushoto ni Ofisa anayesimamia utekelezaji wa Programu wa Taasisi ya Tumaini la Maisha inayohudumia watoto wenye kansa nchini, Lilian Ndyetabula.
Pichani juu na chini baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za MeTL Group jijini, Dar es Salaam.
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Taasisi isiyo ya kiserikali ya MO Dewji iliyo chini ya makampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group) inayojishughulisha na kusaidia jamii imetoa msaada wa Shilingi Milioni 110 kwa taasisi ya Tumaini la Maisha ambayo inajihusisha na kuwasaidia watoto wenye kansa kupata matibabu pamoja kuwahudumia kwa kipindi chote wanachokuwa katika matibabu.
Akizungumzia msaada huo, Afisa Mahusiano wa MO Dewji Foundation, Zainul Mzige alisema kuwa MO Dewji Foundation imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa watoto ambao wanagundulika kuwa na kansa kuja Dar es Salaam kupata matibabu na msaada ambao wameutoa wanataraji kuwa utatumiwa vizuri na taasisi hiyo ili kuzidi kusaidia watoto.
Alisema wameshafanya kazi nyingi na Taasisi ya Tumaini la Maisha na wanawatambua katika utendaji wao wa kazi kusaidia watoto ambao wana kansa na msaada huo wa milioni 110 wanataraji utakuwa na faida kubwa kwa kutumika kusaidia watoto waliopo mikoani na hapa Dar ambao wanakutwa wakiwa na kansa na hivyo msaada huo utasaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi.
“MO Dewji tumekuwa tukisaidia miradi mbalimbali ya kijamii na kama jinsi tunavyosaidia katika miradi hiyo na leo tunafuraha kutoa Shilingi Milioni 110 za kitanzania kwa Tumaini la Maisha tunaamini ni shirika linalotoa matumaini mapya kwa wagonjwa na familia zao,
“Tumekuwa tukishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii tunafahamu ni jinsi gani wanavyosaidia watoto wenye kansa na kama jinsi tulivyokuwa tunashirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kimatibabu na leo tunatoa msaada mwingine ili kuwawezesha kuzidi kuwasaidia watoto hao,” alisema Mzige.
Aidha Mzige alisema kuwa MeTL Group kupitia kwa MO Dewji Foundation wanatambua ni jinsi gani serikali imekuwa ikipambana na ugonjwa huo kwa kuwasaidia watoto wenye kansa na wao wanaahidi kuendelea kuwasaidia kwa kutoa misaada kwa watoto wenye kansa ili waweze kupata matibabu na kuokoa maisha yao.
Awali Afisa Mahusiano huyo alisema kuwa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji aliamua kuanza kuwasaidia watoto wenye kansa baada ya kukutana na mtoto wa miaka 7 aliyetambulika kwa jina la Zakia mwaka 2012 wakati akiwa mbunge wa Singida Mjini ambaye alikuwa akisumbuliwa na kansa ambayo ilikuwa imeshasambaa mwili mzima.
Mzige alisema Dewji baada ya kukutana na mtoto huyo alimchukua na kumpeleka hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu lakini walikuwa wameshachelewa kutokana na kansa kusambaa mwilini na hivyo mtoto huyo kupoteza maisha hali ambayo ilimfanya Dewji kujitoa kusaidia watoto wenye kansa ili waweze kupata matibabu na kwa mapema kabla kansa haijasambaa zaidi.
Nae Gerard Mongera ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha aliishukuru MO Dewji Foundation kwa msaada ambao wanaowapatia kwa kipindi chote ambacho wamekuwa wakishirikiana na kuitaja MO Dewji kama taasisi ambayo imekuwa ikiwasaidia zaidi hivyo kuwa na matarajio ya kuzidi kushirikiana
Mongera alisema msaada umetolewa na MO Dewji Foundation utatumika kuwasaidia watoto hao kupata matibabu na chakula kwa watoto wanaoumwa kansa walio katika hosteli za taasisi hiyo na walezi wanaowasimamia watoto hao kwa kuwanunulia chakula na mahitaji mengine muhimu ambayo yanahitajika kwa watoto hao.
“Tumekuwa tukishirikiana kwa muda mrefu na MO Dewji Foundation na natumia fursa hii kuwashukuru kwa msaada wanaotupatia wamekuwa wakitusaidia kwa muda mrefu na tunawaomba wazidi kuwa na moyo huo wa kuwasaidia watoto wenye kansa ambao wengi wao wanatoka mikoani na kwa kusaidiana nao tunaamini tutaweza kuwasaidia watoto wengi zaidi,” alisema Mongera.
Mongera aliongeza kuwa tangu mwaka 2013 walipoanza kufanya kazi na MO Dewji Foundation wamefanikiwa kuokoa zaidi ya asilimia 50 ya maisha ya watoto ambao wamekutwa na kansa na kutumia fursa hiyo kuyaomba makampuni mengine pamoja na watu binafsi kujitokeza kuisaidia taasisi hiyo ili kuwa na uwezo zaidi ya kuwahudumia watoto ambao wanakuwa wanasumbuliwa na kansa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)