Pages

Nauli Mpya za mabasi ya Mwendo kasi zatajwa

Mabasi yaendayo kwa kasi yanatarajia kuanza kutoka huduma jijini Dar es salaam hivi karibuni huku nauli za mabasi hayo zikiwekwa hadharani kuwa  ni kati ya Sh. 500 hadi 900 kwa safari moja kwa mtu mzima.

Kwa mujibu wa Tangazo la Sumatra kwa vyombo vya habari jana lilieleza kuwa, mamlaka hiyo imepokea maombi ya nauli kutoka kwa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart) ambao utatoa huduma ya usafiri wa umma katika kipindi cha mpito.
Tangazo hilo lilieleza kuwa, safari katika njia kuu pekee mathalani Kimara Mwisho hadi Kivukoni itakuwa Sh. 700 kwa mtu mzima wakati nauli ya mwanafunzi itakuwa Sh. 350. Hivyo kwenda na kurudi kwa mtu mzima itakuwa Sh. 1,400 na mwanafunzi itakuwa Sh. 700.

Aidha, nauli ya pembezoni (Mbezi hadi Kimara Mwisho), itakuwa Sh. 500 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 250.

Safari nyingine ni kwa abiria wanaotumia njia ya pembezoni, njia kuu halafu njia ya pembezoni. Mfano wa safari hiyo ni wanaotoka Mbezi-Kimara Mwisho hadi Morocco; nauli yao itakuwa Sh. 900 na wanafunzi itakuwa Sh. 450.Katika hatua nyingine pendekezo lingine la nauli ni kwa abiria watakaopita njia ya pembezoni na kisha njia kuu kama kutoka Mbezi-Kimara Mwisho hadi Kivukoni, nauli itakuwa Sh. 800 kwa mtu mzima wakati kwa mwanafunzi itakuwa Sh. 400.

Meneja Miundombinu wa Udart, Mohammed Kaganda, amesema wanategemea kuanza rasmi kazi ya usafirishaji wa abiria kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni mapema mwezi ujao.
Alisema mabasi yanayotegemea kuanza kazi katika kipindi cha awali ni 80 na kwamba yatafanyakazi sambamba na daladala za kawaida.

“Katika awamu hii, daladala zitaendelea kufanyakazi kama kawaida lakini hazitatumia njia za mwendo kasi, zitakuwa kwenye barabara hizi za kawaida zinazotumika sasa,” alisema Kaganda.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)