Pages

KESI YA TALAKA YA MMILIKI WA ST. MATHEW YAAHIRISHWA TENA

court_gavel
Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA ya Mwanzo Kizuiani Mbagala, Dar es Salaam, imepanga Septemba Mosi mwaka huu kutoa hukumu katika kesi ya madai ya talaka na mgawanyo wa mali zenye thamani ya Sh Milioni 800 inayomkabili Mmiliki wa Shule ya Sekondari ya St. Mathew na St. Marks, Thadei Mtembei.
Hukumu hiyo ilipangwa kusomwa juzi lakini iliahirishwa kutokana na upande wa mlalamikaji kutofika mahakamani.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Rajab Tamambele alisema kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya hukumu na kwamba itaendelea Septemba Mosi mwaka huu.
Mlalamikaji Magreth Mwangu anaiomba mahakama imuamuru mdaiwa kutoa Sh. Milioni 800 na makazi ya kukaa yeye na watoto wake.
Katika kesi hiyo, upande wa mlalamikaji ulikuwa na mashahidi wanne wakiwamo watoto watatu aliozaa na Mtembei ambao wanasoma katika shule za St Mary’s International na Hijra Seminari ya Dodoma.
Watoto hao walidai kuwa wanasumbuliwa ada shuleni na kwamba wanahitaji malezi yote kutoka kwa baba yao.
Pia waliieleza mahakama kuwa mara ya mwisho kumuona baba yao ni mwaka 2011.
Mtoto wa kwanza wa Mwangu alidai kuwa mwaka 2012 walifika katika Hoteli ya baba yao ya Sleep inn ndipo aliwafukuza na kuwaambia kuwa hawezi kuwalipia ada na badala yake aliwapa Sh 40,000 kila mmoja, fedha ambazo aliziacha mezani.
Pia walidai kuwa Mtembei aliwatolea maneno ya kashfa kwamba hata mama yao aende wapi, anao uwezo na kwamba anajeshi ambalo popote linafika.
Aidha, kwa upande wa mdaiwa, ulikuwa na mashahidi watatu akiwemo Mtembei ambaye alikiri kuzaa na Mwangu na kwamba alitoa ng’ombe watano kama faini ya kuzaa naye.
Mutembei alidai alifahamiana na Mwangu wakati akiwa mfanya usafi katika duka lake la dawa na kwamba hakuwahi kuishi naye.
Hata hivyo, Agosti Mosi mwaka huu, mahakama hiyo ilihamia Singida kwa ajili ya kuthibitisha kama kweli mdai ameuza nyumba ambazo alizijenga pamoja na mdaiwa.
Kiongozi wa msafara huo ni pamoja na Hakimu Tamambele, karani wa mahakama, na ofisa ustawi wa jamii wa mahakama pamoja na mdaiwa, lakini ilidaiwa kuwa hakukuwa na mzee wa baraza ili kuthibitisha.
Aidha mlamikaji huyo alidai kuwa hatendewi haki kutokana na mahakama kusikiliza upande mmoja wa mdaiwa.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)