Pages

Kibiki aikumbuka Lipuli, asema ni agenda yake akipata Ubunge

NA MWANDISHI WETU, IRINGA

MGOMBEA wa nafasi ya Ubunge kwa tiketi ya CCM, Mwanahabari Frank Kibiki ameahidi kushirikiana na wadau wa soka kupandisha daraja timu ya soka ya Lipuli ya mjini Iringa iwapo atapewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza wakati wa kampeni za kujinadi zilizofanyika katika eneo la Kihesa kilolo, mjini Iringa Kibiki alisema michezo ni fursa ambayo inaweza kuinua uchumi wa mkoa wa Iringa endapo itapatiwa kipaumbele.

Alisema ikiwa atapewa ridhaa ya kuwa mbunge, atakaa chini na wadau wa soka wa manispaa ya Iringa na kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wananchi Lipuli inapanda daraja.

“Ndugu zangu, Lipuli ikipanda daraja uchumi wa Iringa mjini utakuwa kwa sababu vijana watapata ajira kwa sababu kwenye uwanja wetu wa samora, zitachezwa timu za kimataifa,” alisema Kibiki.

Aidha alisema kuwa ataimarisha timu nyingine za mjini Iringa ili ziweze kupanda madaraja sambamba na kuinua sekta ya sanaa hasa muziki.

Katika hatua nyingine, Kibiki aliwashauri vijana  kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali na kutumia  fursa zilizopo kwenye  maeneo yao ili waweze kujiajiri na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Kibiki alisema, umoja ni nguvu na ikiwa vijana watajiunga kwenye vikundi hivyo vya kiujasiriamali itakuwa rahisi kufanikiwa kiuchumi.

Alisema maeneo mengi ambayo vijana wameungana wameweza kukopeshwa, na wanaendesha shughuli zao za kiuchumi bila wasi wasi, jambo hilo linawezekana.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)