Pages

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA) YAZUNGUMZIA MAFANIKIO NA MIRADI YAKE MBALIMBALI

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Suleiman Suleiman, akizungumza na waandishi wa habari katika banda la mamlaka hiyo kwenye maonyesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAA pamoja na miradi yao.
 Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Laurent Mwigune (kulia), akizungumza na wanahabari kuhusu shughuli zinazofanywa na TAA.
 Kamanda Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Kamishna Msaidizi, Mpemba Magogo (katikati), akizungumza na waandishi habari kuhusu kazi za uokoaji pale unapotokea moto. Kulia ni Koplo, Brian John wa Kikosi hicho cha Zimamoto.
 Koplo, Brian John wa Kikosi hicho cha Zimamoto katika uwanja huo akionyesha zana zake za kazi za kuzimia moto.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Suleiman Suleiman (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wake kwenye banda lao.
 Wafanyakazi wa idara mbalimbali wa TAA wakiwa katika picha ya pamoja katika maonyesho hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Suleiman Suleiman akiondoka baada ya kuzungumza na wanahabari.

Na Dotto Mwaibale

MAMLAKA  ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema  upanuzi wa jengo la tatu wa awamu ya pili katika viwanja vya ndege nchini unatarajia kukamilika mwakani, utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 7.5 kwa siku.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo asubuhi na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleiman Suleiman, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Alisema mwanzoni viwanja hivyo vilikuwa na uwezo wa kuchukua watu milioni 1.5 kwa siku, lakini kwa sasa uwezo wake ni watu milioni 2.5, hivyo kukamilika kwa mchakato huo kutarahisisha kusafiri kwa urahisi kwenda sehemu yoyote ya nchi iwe ndani na nje.

"Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza utaufanya kuwa wa kimataifa, ndege zitakuwa zikitoka Mwanza na kwenda Ulaya hadi mataifa mengine, itapunguza gharama za usafirishaji na kumsaidia mwananchi wa kawaida kumudu gharama," alisema.

Aliongeza, ili kudhibiti uingizwaji wa madawa ya kulevya katika viwanja vya ndege, wameweka kamera maalumu zitakazosaidia kutambua mizigo ambayo si salama.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Kikosi cha  Zimamoto na Uokoaji katika viwanja hivyo, Mpemba Magogo, alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa, usalama upo katika maeneo hayo, hivyo wasiwe na hofu.

Alisema kuna baadhi ya changamoto kama kukua kwa teknolojia hivyo, inatakiwa uwanja huo kuwa na vifaa vya kisasa vya kutosha. 

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)