Pages

Rais wa Zanzibar, Dk Shein afunga mkutano wa mabalozi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania

Balozi Seif kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein akiufunga Mkutano wa Nne wa siku Tatu wa Mabalozi wa Tanzania uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Ramada Mjini Dar es Salaam.Baadhi ya Mabalozi wa Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani walioshiriki Mkutano wao wakifuatilia Hotuba ya Ufungaji wa Mkutano huo iliyosomwa na Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. ASli Mohammed Shein.Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wa Tanzania Nchi mbali mbali Duniani mara baada ya kufunga Mkutano wao wa Nne ulifanyika Ramada Hoteli Jijini Dar es Salaam. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mh. Bernard Membe, Katibu Mkuu Mpya wa Wizara hiyo Balozi Lebereta Mula mula na kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mhadhi Juma Maalim. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Abrahaman Nyimbo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Mabalozi wa Tanzania Mjini Dar es salaam. Picha na – OMPR – ZNZ. 
---
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema Mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania katika Mataifa tofauti Duniani wanapaswa kuitekeleza vilivyo Sera ya Mambo ya Nje inayolenga katika Diplomasia ya uchumi ambayo ndiyo muongozo wao katika utekelezaji wa jukumu lao la msingi.

Alisema Sera hiyo ni vyema ikatumika vizuri wakati huu ambao Taifa la Tanzania linatekeleza Dira ya kuelekea uchumi wa Kati na kati ifikapo mwaka 2020 kwa upande wa Zanzibar na Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara.

Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akiufunga Mkutano wa Nne wa siku Tatu wa Mabalozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Ramada Jijini Dar es Salaam.

Alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye kuweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi Tanzania imepiga hatua kubwa vikiwemo Visiwa vya Zanzibar.

Dr. Shein alifahamisha kwamba matunda ya Sera hii yanadhihirisha wazi ukuaji wa sekta ya Utalii, miradi mengine ya kiuchumi ikiwemo pia ile mikubwa inayotekelezwa na wahisani kwa upande wa Zanzibar.

“ Mikakati mipya ya muda mfupi na mrefu mliowekeana katika Mkutano huu ni msingi mzuri kabisa kufuatana na mabadiliko ya uchumi yanayotokea Duniani na kufikia malengo ya Dira ya 2020 na 2025 “. Alisema Dr. Shein.

“ Nina hakika kuwa katika Mkutano huu mmeweza kuziba nyufa zote zilizojitokeza katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 inayolenga katika Diplomasia ya Uchumi ambayo ndio muongozo wetu katika utekelezaji wake na ni jukumu letu la msingi “. Alisisitiza Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba licha ya mafanikio makubwa ya kiuchumi na maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa kwa upande wa Zanzibar lakini bado iko haja kwa Mabalozi hao wa Tanzania kuongeza juhudi za kuitangaza Zanzibar katika Mataifa waliyopangiwa kutekeleza majukumu yao ya Kidiplomasia.

Alisema mafanikio ya Zanzibar katika kukuza sekta ya Utalii , uwekezaji na utekelezaji wa mipango mengine ya maendeleo hutegemea sana juhudi za Ofisi za Kibalozi katika kuitangaza Zanzibar nchi za Nje.

Dr. Shein alifahamisha kwamba baadhi ya wakati Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wawekezaji, watalii na wageni wanaofika Zanzibar juu ya ukosefu wa taarifa za kutosha kuhusu Zanzibar katika Ofisi za Kibalozi za Tanzania.

Aliwakumbusha Mabalozi hao kwamba katika kutekeleza majukumu yao ni vyema kila wakati wakazingatia kuwa Ofisi zao zinaweka taarifa za kutosha juu ya sekta zote muhimu za kiuchumi na kijamii za pande zote mbili za Jamuhuri hasa zile fursa za uwekezaji vivutio vya utalii.

“ Suala hili nimekuwa nikilikumbusha kila ninapopata fursa ya kuzungumza nanyi, hasa wakatia mbao Mabalozi huja kunitembelea na kuniaga kabla ya kuripoti katika vituo vyao vya kazi “. Alifafanua Dr. Shein.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kupokea mawazo ya Mabalozi hao ili kupata fursa nzuri ya nini Wanadipomasia hao wakitangaze kuhusu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar alihimiza kwamba katika kipindi hichi ambapo Nchi mbali mbali Duniani zimekumbwa na misukosuko ya kutetereka kwa hali ya amani na utulivu Mbalozi hao wanapaswa kuzitangaza fursa ya kiuchumi zilizopo Nchini na kuzihusisha na hali ya amani na utulivu uliopo Nchini Tanzania.

Alieleza kuwa amani na utulivu ni miongoni mwa vigezo muhimu vya awali vinavyozingatiwa na wawekezaji pamoja na wageni wanaotaka kwenda nje ya nchi zao kwa nia ya kuwekeza na kufanya biashara.

Mapema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Mh. Bernard Membe alisema utekelezaji wa sera ya mambo ya nje inayolenga katika Diplomasia ya Uchumi umeleta faida kubwa katika uchumi wa Taifa ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Waziri Membe alisema ipo miradi kadhaa ya kiuchumi iliyotokana na sera hiyo kufuatiwa kutanganzwa na Ofisi za Kibalozi za Tanzania akiitaja kuwa ni pamoja na misaada ya maendeleo iliyofadhiliwa na mpango wa Milenia wa Marekani MCC na mradi wa chuma wa Mchuchuma.

Mh. Membe alisisitiza pia kuwa ipo miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Tanzania kusamehewa mikopo tofauti kutoka kwa baadhi ya wafadhili, mradi wa huduma za maji safi unafadhiiwa na Serikali ya Japan pamoja na mradi wa Kilimo kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya nje itahakikisha kwamba inaendelea kuchangia vikosi vya kulinda amani Barani Afrika.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa Mkutano huo wa Nne wa Mabalozi wa Tanzania Nchi Mbali mbali Duniani Dini wa Mabalozi hao Balozi Kijazi alisema Maalozi hao wakirudi vituoni mwao watakuwa na kazi moja tu ya kutekeleza yale waliyoyajadili na kukuibaliana katika Mkutano huo.

Balozi Kijazi alilihakikishia Taifa kwamba Mabalozi hao wana nia safi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufasini uliotukuka, lakini lakuzingatia zaidi ni uwezeshwaji wao ili kutekeleza vyema kazi yao hiyo ya Kidiplomasia.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)