Pages

Mgomo wa mabasi waendelea kutikisa

 Mabasi yakiwa yameegeshwa Kituo cha Mabasi Ubungo baada ya madereva kuwa katika mgomo wa kimasilahi Dar es Salaam jana. Mgoma huo umefanyika nchi nzima ukihusisha na daladala hivyo kuleta adha kwa wananchi.
 Wananchi wakitembea maeneo ya Jangwani kutokana 
na mgomo huo.
 Wanafunzi na watu wengine wakitembea maeneo ya chuo cha maji Ubungo wakielekea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
 Hali ilivyokuwa stendi ya Ubungo.
 Baadhi ya madereva, wapiga debe na makondakta wakikimbia huku wakiimba wanaonewa na wanataka mikataba ya kazi zao .
 Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), wakiimarisha ulinzi maeneo yanayozunguka kituo hicho cha mabasi cha ubungo.

 Wananchi wakisubiri mabasi kwenye kituo cha Makumbusho

 Kituo cha mabasi cha Makumbusho kikiwa hakina mabasi kutokana na mgomo huo.
 Askari wa FFU wakiwa doria maeneo ya Ubungo Mataa.
Madereva, wapiga debe na makondakata wakishangilia jambo wakati wakiongea na viongozi wao kuhusu mgomo huo.

Dotto Mwaibale

MADEREVA wa mabasi na daladala wamesema wapo tayari kula biskuti wakati wakiendelea na mgomo wao ulianza rasmi jana mpaka  hapo serikali itakapokaa nao ili kuumaliza mgpmo huo.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam leo asubuhi na  Makamu mwenyekiti wa Umoja wa Madereva, Shabani Mdemu kati akizungumza na wanachama wa umoja huo na wadau wengine.

"Tupo katika wakati mgumu sana lakini tupo tayari kula biskuti lakini hatuta rudi nyuma ni vema tukae katika hali hii kwa siku mbili na zaidi mpaka tupate majibu ya kueleweka" alisema Mdemu.

Mdemu alisema haoni kwanini viongozi wenye dhamana wanashindwa kufika kuzungumza hana hana na wanachama hao badala ya kwenda maofisi kwao baadhi ya viongozi tu.

"Wanapotafuta kura huwa wanaenda vijijini kuomba sasa wanashindwa nini leo hii kutufuata hapa tulipo kuja kusikiliza kilio chetu" alisisitiza Mdemu huku akishangiliwa na wanaumoja hao.


Akizungumzia kuhusu kutatua mgogoro huo Mdemu alisema walimuomba waziri mkuu afike za kufika kutokana na hali ya usalama katika eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo madereva hao walipinga vikali kitendo cha waziri kuwataka wamfuate hivyo waliamua kuendelea kugoma hadi hapo Waziri atakapoamua kufika.

"Tumemuomba Waziri aje kusikiliza kilio chetu lakini amesema hawezi kuja kutokana na hali ya kiusalama hivyo sisi tunaenelea kugoma hadi atakapoamua kuja kutusikiliza.

"Kuna mambo mengi ambayo Waziri alituahidi atatutekelezea kipindi kile cha mgomo wa mwanzo lakini hadi sasa hayajatekelezeka na ndiyo maana leo hii tunagoma," alisema

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, aliwasili eneo la tukio tangu majira ya saa 12 asubuhi akiwa na kikosi chake kwaajili ya kuangalia usalama katika eneo hilo.

Lakini ilipofika majira ya saa 3:30 asubuhi aliamua kuondoka huku akidai kuwa hana chochote ambacho angeweza kuzungumza kwani viongozi wapo katika mazungumzo.

Kamanda Mpinga alisema kuwa hana chochote cha kusema kwani atarudia yale yale na kuwataka madereva wamsubiri Waziri Mkuu Mizengo Pinda hadi majira ya saa sita kwaajili ya mazungumzo na madereva hao.

Kadri muda ulivozidi kwenda hali ilizidi kuwa tete kutokana jambo ambalo lilipelekea kuongezeka kwa vikosi vya jeshi la polisi huku wakitumia mabomu ya machozi na mbwa.

Lakini hadi kufikia majira ya saa sita mchana hakuna kiongozi wowote wa serikali waliofika eneo hilo, huku madereva wakiwa wameegesha mabasi yao na wasafiri wakiwa hawafahamu hatima yao.

Hata hivyo mmoja wa askari polisi ambaye ni trafiki aliyejulikana kwa jina la Solomon Mwangamilo alizua taharuki katika eneo hilo alipotaka kutoa Bus lililokuwa likielea mwanza lijulikanalo Lucky Star.

Hali hiyo lisababisha madereva kumzomea na kutanda mbele ya gari huku na kulizuia gari hiyo kutoka , madereva hao walifanikiwa na gari hilo liliridishwa ndani ya stebi ya Ubungo.

Aidha moja ya madereva wa magari hayo Ngonyani Gervas alisema wamechoka kunyanyaswa tunataka haki zetu kama madereva pia tunataka wawakilishi wetu bungeni.

"Mbona fani nyingine zina  wawakilishi bungeni na sisi madereva tumechoka tunataka wawakilishi bungeni kama ilivyo kwa vyama vingine kama albino kwani hii fani haitambuliki kitaifa?  "

Aliongeza kuwa Kama viongozi wameshindwa kuwasaidia  katika fani yao taaluma hiyo ifutwe.

Kwa upande wake Msemaji wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Gervas Rutavunzinda, alisema Katiba ya nchi inamruhusu mtu kusafiri kutoka sehemu moja kenda nyingine, na huu mgomo umevunja katiba kwani ni kuwakosesha abiria haki yao ya kusafiri.

Alisema abiria anakuwa amekidhi vigezo anapokata tiketi lakini akishindwa kusafiri inakuwa ni tatizo la mmiliki na serikali hivyo tatizo hilo linatakiwa kuingiliwa kati na serikali ili kuondokana na mgogoro.

"Kitendo cha kumrudishia abiria nauli kunakuwa umemnyima haki kwasababu abiria wengi wamekuwa wamejiandaa halafu anashangaa anafika sehemu husika kwa ajili ya safari unamwambia ahirishe safari jambo ambalo si zuri.

"Hili tatizo ni la wamiliki na madereva haliwahusu abiria, serikali inapaswa kuangalia tatizo lilipo na kuhakikisha halitokei tena pia mamlaka husika zihakikishe zinatatua matatizo kama hayo kutokana na madhara kuwa makubwa," alisema.

Katika hali isiyo ya kawaida kulitangazwa kurudishwa nauli kwa abiria ambao wapo hiari kuahirisha safari zao lakini madereva hao walishindwa kufanya hivyo kutokana na fedha hizo kupelekwa kwa wamiliki na kufanyiwa manunuzi ya mafuta ya magari hayo kwa kuanza safari.

Mmoja wa Utingo wa Basi la Majinja Express linalofanya safari zake Dar Mbeya Sumbawanga Flora Ngailo alisema kitendo cha kurudisha nauli kwa abilria hao hakitawezekana kutokana na fedha hizo wameshamkabidhi mmiliki na tayari zimeshanunuliwa mafuta.

"Hatuwezi kurudisha fedha za nauli hizo kwasababu tayari mahesabu yameshaenda kwa bosi na zimeshanunuliwa mafuta, labda wasubiri hadi hapo tutakapopewa taarifa za kuondoka au waahirishe hadi kesho asubuhi," alisema Ngailo.

Kwanyakati tofauti abiria waliokuwa wakitaka kusafiri kituoni hapo Rehema Obadia na Issa Jafari, walisema mgomo huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa kwani mamlaka ilitakiwa kutoa taarifa kwa wananchi kama kutatokea kwa mgomo huo.

"Mamlaka husika walitakiwa kutoa taarifa kwa wananchi kuwa kutatokea hali kama hii, sasa hivi hatujui tutasafiri au hatutasafiri kwani hakuna lolote yunaloambiwa,

"Hatuna taarifa zozote hadi sasa hatujala tuna watoto, wagonjwa na hutujanywa chai na wengine wamefiwa hadi sasa hali hii inasababisha kuingia gharama upya na hatujui hatma yetu," alisema.

"Huu ni uzembe wa serikali kwani walipaswa wasikatishe tiketi kwasababu mgomo huu wanaujua na hii ni sanaa ya wanafanya, serikali watatue migogoro kama hii kwa wakati ili kuepusha adha kama hizi," walisema.

Vituo vya daladala

Katika kituo cha daladala Makumbusho hapakua na gari ya abiria bali kulikuwa na magari binafsi, Bajaji na Pikipiki zilizokuwa zikitumika kubebea abiria.

Kituoni hapo palikuwa na abiria ambao walikuwa hawajui hatma ya safari yao na ni namna gani wataenda makazini wengine wakilalamika kuchelewa vipindi vyuoni kutokana na kutokuwepo kwa usafiri eneo hilo.

Mmoja wa abiria, Diana Bernard alisema mgomo huo umemuathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli zake kukwama ikiwa ni pamoja na kushindwa kuelekea chuoni.

Hadi waandishi wa gazeti hili wanaondoka eneo la ubungo bado hakukua na dalili yoyote ya ujio wa Waziri Mkuu badala yake madereva hao walikuwa mameshikilia kuwa msimamo wao kuwa mgomo upo palepale.

Waziri wa Kazi na Ajira.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka aliwataka madereva kuachana na migomo hiyo kwani serikali inafanyia kazi madai  yao hivyo wawe wavumilivu.

"Wao wanasema kuwa wanadharauriwa lakini si kweli kwani tulikaa pamoja tukaelewana na hivyo tunayafanyia kazi madai yao na mambo yatakuwa mazuri tu"alisema




 (Imeandaliwa na mtandao wa http://www.habarizajamii.com/)

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)