Pages

Assumpter akimbilia kwa Kinana kulinda jimbo

ASSUMPTER Mshama-Mbunge wa Nkenge (CCM), amekimbilia kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, akiwashtaki makada wenzake watano kwamba wameanza kampeni ya kumnyang’anya jimbo mapema. Anaadika Edson Kamukara … (endelea).
Mbunge huyo anakuwa wa pili kuomba huruma ya Kinana asing’olewe kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni. Aliyetangulia ni Mbunge wa Tabora Kaskazini, Sumar Shaffin Ahmedali, ambaye  anamtuhumu Almasi Athumani Maige, kuanza kampeni kabla ya wakati na kinyume cha taratibu.
MwanaHALISIOnline limeona barua hiyo ya Assumpter ya 24 Machi 2015, ambapo anawataja; mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Deodorus Kamala, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Aidal Kamugunda, Julius Rugemala, Joachim Mazima na Kyombo anayetajwa kwa jina moja.
Assumpter anasema “Matendo tajwa hapo juu yameleta mvurugano ndani ya chama chetu katika ngazi za kata na Wilaya ukizingatia kuwa muda wa kufanya hivyo bado. Kama ulivyoelekeza awali kwa wagombea urais, kuwa ambao watafanya kampeni kabla ya wakati watapoteza sifa, vivyo hivyo naomba chama kinisaidie kutoa mwongozo katika jimbo langu kufuatia matukio haya ya kampeni za ubunge kabla ya wakati.”
Wachambuzi wa siasa ndani ya CCM katika jimbo hilo, wanasema upepo unamvumia vibaya Assumpter. Wanasema “hata kukimbilia kwa Kinana ni bure kwani akipitishwa huenda akaanguka kwa Chadema.
Kupitia barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosomeka; “wagombea ubunge waliofanya kampeni kwa kufanya za kibunge kabla ya wakati”, Assumpter anasema “Kwa masikitiko makubwa, ninapenda kuifahamisha ofisi yako kuwa, tangu mwezi Januari mwaka huu 2015 kumekuwepo wimbi kubwa la watu ambao ni wanachama wa CCM walioazimia kugombea ubunge katika jimbo ninaloliwakilisha sasa la Nkenge.
“…watu hawa wamekuwa wakifanya mikutano ya hadhara yenye lengo la kunishusha kisiasa, kuandaa vyakula na kualika watu wengi ambao pia wamekuwa wakigawiwa fedha kati ya elfu kumi mpaka ishirini na zaidi. Walengwa hasa katika mialiko na mgao wa fedha hizo ni makatibu wa vyama wa kata na viongozi mbalimbali wa kata katika chama chetu.” 
Anasema kuwa makada hao wamekwenda mbali zaidi kwa kuanza kampeni moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kufanya kazi za kibunge kwa kuchangia mifuko ya saruji na mabati, kupeleka malori ya mchanga na kutengeneza barabara katika maeneo yenye mahitaji kwa wananchi.
Mbunge huyo analalamika kuwa, “haya yanafanyika kwa kisingizio cha kuchangia maendeleo lakini sivyo. Kama yangefanyika bila shutuma dhidi yangu, ingeeleweka lakini sitendewi haki kwa kumwagiwa shutuma hadharani hali wananchi wakipozwa na misaada yenye ajenda za siri.”

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)