Pages

Mbaroni kwa mapenzi mchezaji Sunderland

Adam Johnson mchezaji wa Sunderland ya England
Mchezaji wa timu ya taifa ya England ambaye pia anakipiga katika klabu ya soka Sunderland Adam Johnson amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na msichana mwenye umri wa miaka 15. Polisi katika eneo la Durham wamesema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amekamatwa mapema wiki hii kwa tuhuma za kufanya ngono na binti mwenye umri wa chini ya miaka 16, na amebaki chini ya ulinzi. Taarifa ndani ya klabu yake zinasema kuwa mchezaji huyo amesimamishwa kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi. Taarifa za kukamatwa kwake zilitolewa mapema kupitia gazeti la The Sun. Kukamatwa kwake kunakuja muda mfupi kabla hajasafiri na timu yake ya Sunderland kwenda kukutana na Hull kwa michezo ya Ligi kuu ya England iliyopangwa kuchezwa leo usiku. Sunderland imesema haitaendelea kuzungumzia kukamatwa kwa mchezaji wake.
Wachezaji wa Azam ya Tanzania
Katika ligi kuu ya Italia maarufu kama Serie A iliendelea tena usiku wa kuamkia leo kwa kushuhudiwa mchezo mmoja wa kukata na shoka. AS Roma walikuwa wenyeji wa vinara wa ligi hiyo Juventus katika dimba la Olympic na hadi mwisho wa mtanange huo matokeo yalikuwa sare ya 1-1. Juventus bado ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 58 wakati nafasi ya pili ikibaki kwa AS Roma.
Nako nchini Tanzania, timu ya Azam iliyokuwa ikishiriki michuano ya klabu bingwa barani Afrika, imemtimua kocha wake Mcameroon Joseph Omog baada ya kutolewa katika mashindano hayo pale ilipochapwa mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano na El Mereikh nchini Sudan mwishoni mwa wiki. Azam ilishinda mchezo wa kwanza dhidi ya El Mereikh kwa kuicharaza mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita. Azam iliyaaga mashindano hayo kwa kuchapwa jumla ya magoli 3-2.Chanzo BBC Swahili

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)