Pages

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU YAMPA ONYO JOSEPH LUDOVICK

Picture
Mtuhumiwa namba mbili Joseph Ludovick (kulia) wa kesi ya kula njama za kutaka kumteka na kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, akitoka nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam jana baada ya kuachiwa kwa dhamana. Kushoto ni rafiki yake, Hamfrey Masawe. (Picha na Venance Nestory)
NA FLORA MWAKASALA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemwonya mshitakiwa mwenza wa Mkurugenzi wa Ulinzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, Ludovick Joseph, kutozungumza na vyombo vya habari wala mitandao ya kijamii. Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, alitoa onyo hilo jana baada ya Wakili Nyaronyo Kicheere, kulalamikia kitendo cha mshitakiwa Joseph kuzungumza na waandishi wa habari na kuchapisha habari za kesi hiyo magazetini.


Kutokana na malalamiko hayo, Hakimu Katemana alimtaka Joseph kutozungumzia kesi hiyo kwenye vyombo vya habari, kwa sababu si utaratibu na akiendelea kufanya hivyo atafutiwa dhamana.Wakati huo huo, Mahakama hiyo imetoa kibali kwa Lwakatare kwenda kutibiwa mgongo nje ya nchi.

Awali Wakili Kicheere aliiomba Mahakama itoe kibali kwa Lwakatare, ili aende nje kutibiwa matatizo hayo yanayomsumbua. Aliwasilisha nyaraka zilizotolewa na Daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuonesha kuwa Lwakatare anasumbuliwa na tatizo hilo na anatakiwa aende nje ya nchi kupata matibabu.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Katemana, ambapo upande wa mashitaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Ponsiano Lukosi huku Lwakatare akiwakilishwa na Wakili Kicheere.

Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, na washitakiwa hao wanaendelea kuwa nje kwa dhamana, hadi Agosti 21 itakapotajwa tena. Hivi karibuni baada ya kupata dhamana, Ludovick aliomba kupitia mtandao wa kijamii wa Mabadiliko, ahojiwe na waliotaka kujua zaidi kuhusu kesi yake.

Baada ya kuhojiwa huku akijibu maswali ya waliomhoji, gazeti la Mtanzania lilichapisha sehemu ya mahojiano hayo na kumfanya Kicheere aombe mshitakiwa huyo kuzuiwa kuzungumzia kesi hiyo nje ya mahakama.

Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama kwa nia ya kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.

CHANZO:HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)